
Ni dhahiri sasa vyama vya Chadema na ACT-Wazalendo vimeanza kuumana jino kwa jino kutokana na kupishana kwenye mikutano ya kisiasa inayoendelea mikoani.
Wakati vyama hivyo vikiendelea kuchuana na kujaza mamia ya wananchi
kwenye mikutano yao, viongozi wake wamekuwa wakituhumiana kwa mambo
mbalimbali.
Vyama hivyo vimekuwa vikipishana katika kanda tangu vilipoanza ziara za
mikoani hivi karibuni. Wakati Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, John
Mnyika akiwa mkoani Mtwara, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe
alikuwa mkoani Ruvuma na timu yake.
Baada ya Mnyika kumalizia ziara hiyo, alirejea Dar es Salaam kabla ya
kuanza mikutano yake Kanda ya Ziwa, ambako ACT nao walikwenda.
Akiwa mkoani Mwanza mwishoni mwa wiki, Mnyika akihutubia mamia ya
wananchi kwenye viwanja vya Furahisha, alisema Chadema haiko tayari
kuwakaribisha ACT-Wazalendo kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Lakini siku moja baada ya Mnyika kuondoka Mwanza, Zitto na msafara wake nao waliwasili mkoani humo.
Baada ya kuwasili, Zitto alifanya mkutano wa hadhara kwenye viwanja
hivyo hivyo na kusema ACT-Wazalendo wamejipanga kurudisha uzalendo.
Baada ya mkutano huo, jana Zitto aliwasili mkoani Mara ambako alifanya mkutano mkubwa wa hadhara.
Alisema kamwe hatorudi nyuma kwa maneno ya watu, kwani safari ya mapambano imeanza.
Zitto alisema hivi sasa kuna kundi la watu waliojivika upinzani dhidi ya
ACT-Wazalendo, ambao wamekuwa wakikesha ili waone chama hicho kinapotea
katika siasa za nchi hii.
Akizungumza katika mkutano huo kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Mukendo
mjini Musoma, Zitto alisema ameamua kuingia kwenye jahazi la ACT, huku
akitambua namna ambavyo anapigwa kila aina ya mishale na watu
wasiomtakia mema kwenye siasa.
Alisema anashangazwa na madai ya watu hao kueneza kila aina ya
propaganda zenye lengo la kukiua chama cha ACT-Wazalendo, ikiwamo
kukihusisha na mipango ya kuwaandalia nafasi baadhi ya makada kutoka
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili wagombee urais katika uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, baada ya kutemwa.
“Mimi ndugu yenu nimepigwa mishale mingi kweli ndani na nje – huko
nilikotoka, ikafika mahali unajitahidi kueleza kile unachojua, wenzako
hawakutaki, mngekuwa ninyi mngefanyaje?
“Tumeanza ziara hii baada ya kuona moto wa ACT-Wazalendo umekuwa mkali
na hauwezi kuzimika, wamegeuka na kuanza kusema eti tunawaandalia akina
Edward Lowassa kuja kugombea urais… jamani hilo halipo.
“Hao ambao wamekuwa wakipita kila kona kueneza propaganda za kipuuzi
wajue sasa safari imeanza ya kujenga demokrasia imara na yenye matumaini
mapya kwa upinzani, ACT tunahitaji kujenga taifa imara ambalo lina
misingi ya maadili kwa viongozi wake,” alisema Zitto.
Akizungumzia ni wapi chama hicho kinapata fedha za kuendesha shughuli
zake, Zitto alisema wanaotakiwa kujibu swali hilo ni wale wanaoeneza
propaganda chafu dhidi yake.
“Waulizwe akina Ediwn Mtei (mwasisi wa Chadema) na Freeman Mbowe
(mwenyekiti) walitoa wapi fedha za kujenga Chadema kabla ya sisi kuingia
na kukijenga hadi kupata ruzuku. Huko walikopata wao ndio njia hizo
hizo napita kuijenga ACT.
“Nimekuwa mbunge miaka 10, nimejenga watu wanaoamini siasa zangu ndani
na nje ya nchi. Sisi ziara yetu mkoa mmoja ni shilingi milioni 3.6 tu.
Je, Zitto anakosa watu 11 wa kila mtu kuchangia mkoa mmoja?” alihoji
huku akishangiliwa.
Zitto alitumia mkutano huo kueleza namna ACT-Wazalendo ilivyojipanga
kuhakikisha inaweka misingi ya nchi na si kuzungumzia siasa zilizopita.
Akizungumzia idadi ya wanachama waliojiunga na chama hicho hadi sasa,
Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano wa ACT-Wazalendo, Msafiri Mtemelwa,
alisema hadi sasa wamefanikiwa kuvuna wanachama wapya 4,610.
“Jana (juzi) tukiwa Mwanza tumefanikiwa kupata wanachama wapya 742,
ingawa mpaka sasa Mkoa wa Tabora unaongoza kwa kuwa na wanachama 815.
“Dodoma 649, Shinyanga 1,104, Singida 594, Ruvuma 528, Njombe 26, Mambako 228, Iringa 471 na Morogoro 1,401,” alisema Mtemelwa.
John Mnyika
Naye Mnyika akihutubia wakazi wa mji wa Musoma kwenye uwanja wa Shule ya
Msingi Mukendo juzi, aliwataka wapenda mabadiliko kumpuuza Zitto kwa
kile alichokidai kuwa ni msaliti na hana uzalendo.
Mnyika alisema Zitto ndiye aliyekuwa akiratibu majimbo ambayo CCM
ilipita bila ya kupingwa kwa kula njama za kuwaondoa wagombea mwaka
2010.
Alisema miongoni mwa majimbo hayo ni pamoja na Mlale linaloongozwa na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Bumbuli linaloongozwa na Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba na Musoma Vijijini
linaloongozwa na Nimrod Mkono.
Mnyika alisema Zitto alifanya usaliti wa kuwaondoa wagombea ili wagombea wa CCM wapite bila kupingwa.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka Watanzania waendelee kuiamini Chadema na Ukawa ili kupata mabadiliko ya kweli.
BOFYA LIKE UJIUNGE NASI MOJA KWA MOJA
BOFYA LIKE UJIUNGE NASI MOJA KWA MOJA
BOFYA HAPA KWA KUJIUNGA NASI MOJA KWA MOJA NA LIKE PAGE YETU
HII NI MO DESIGN
Post a Comment
Tafadhali, Usitumie lugha ya matusi! Maoni yako ni ya muhimu sana kwetu.