KAZI imeanza! Baada ya
ukimya wa muda mrefu uliotokana na Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani,
sasa makamanda wa Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ imeingia kazini ambapo
wiki hii imeweza kuinasa nazi ikiwa na karatasi lenye majina ya
waliojitokeza kugombea urais, ubunge na udiwani kwenye uchaguzi mkuu
ujao.
Tukio la aina yake, lilinaswa kwenye
Makaburi ya Mwananyamala, Dar ambapo OFM walikuwa katika pitapita zake
za kusaka matukio ya kila siku.
Wakati OFM wakikatiza eneo hilo, baadhi
ya wakazi wa eneo hilo walikuwa wakitoka makaburini hapo saa nne asubuhi
huku gumzo likiwa ni akina nani wamethubutu kufika kwenye makaburi hayo
na kutupa nazi hiyo iliyopasuliwa kidogo na karatasi lake pembeni.
“Unajua hawa ni wapambe tu. Si wao
wenyewe. Mgombea urais gani anaweza kuja hapa makaburini Mwananyamala
kutupa nazi na karatasi lenye majina ya wagombea wote hawa. Ili iweje
kwanza?
“Inawezekana kuna kundi la watu ndiyo
wameamua kufanya vile kwa sababu ya ushirikina wao. Lakini inatisha.
Uchaguzi wa mwaka huu jamani, acheni tu,” alisikika akisema mkazi mmoja
wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Zubeda Hassan.
OFM ilitia timu kwenye makaburi hayo na
kushuhudia uchawi huo ambapo nazi hiyo ilikuwa na majina ya wagombea
urais, lakini pia karatasi ilionesha majina hayo sanjari na ya wagombea
ubunge na udiwani wa vyama mbalimbali ambao wengi wao wameanguka katika
kura za maoni.
Wakati OFM inapiga picha, mwanaume mmoja
aliyekataa kujitambulisha jina alifika na kuwatimua akisema kuwa, yeye
ndiye mwenye dhamana ya kuamua nani apige picha na nani asipige na
kwamba watu waliotupa vitu hivyo hapo walisema wangerudi kesho yake
kuangalia kama kazi ilifanyika au la! (hakusema ni kazi gani).
Wakati viashiria vya uchawi kwenye
makaburi hayo yakiishia hivyo, Afisa Habari wa Klabu ya Yanga ya jijini
Dar, Jerry Muro naye hivi karibuni alijikuta katika wakati mbaya baada
ya kudai kuandamwa na mambo ya kilozi kufuatia vijana wawili kuvunja
nazi na mayai mbele yake wakati akitangaza nia ya kugombea ubunge katika
Jimbo la Kawe kwa leseni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Tukio hilo lilijiri wakati wa zoezi la
wagombea kujinadi kwa wapiga kura kwenye Uwanja wa Mabatini Kata ya
Msasani, Dar, majira ya saa 5:00 asubuhi.
Akizungumzia tukio hilo, Jerry aliwaambia OFM kuwa, ishu hiyo ilimshtua na kudai kuwa siasa za aina hiyo zinatia shaka.
“Baada ya wenzangu kama 20 kumaliza
kutoa sera zao, ilipofika zamu yangu. Wakati najieleza ndipo waliibuka
vijana wawili na kuvunja nazi mbili na mayai mbele yangu.
“Ni jambo la fedheha na kunisikitisha
sana, tuombeane ndugu zangu hali yangu ni tete kwani huu ni ushirikina
wa waziwazi,” alisema Jerry.
Hata hivyo, vijana hao walikamatwa na kupelekwa kwenye Kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar kwa maelezo zaidi.
Waandishi: Mayasa Mariwata, Shani Ramadhani na Gabriel Ng’osha.
BOFYA HAPA KWA KUJIUNGA NASI MOJA KWA MOJA NA LIKE PAGE YETU
HII NI MO DESIGN
Post a Comment
Tafadhali, Usitumie lugha ya matusi! Maoni yako ni ya muhimu sana kwetu.