Makongoro Oging’ na Haruni SanchawaHALI bado ya majonzi! Watu bado wanalia, hususan wakazi wa maeneo ya Buguruni, Ilala jijini Dar es Salaam kufuatia vifo vya watu tisa wa familia moja vilivyotokana na kuteketea kwa moto uliozuka saa tisa usiku wa Agosti 13, mwaka huu kwenye nyumba ya mzee Masoud Mattar Masoud ambaye siku hiyo ya tukio alikuwa kazini bandarini.
Muonekano wa nyumba hiyo baada ya kuwaka moto.
nauma sana na simulizi yake inatisha! Familia imefutika kabisa katika uso wa dunia, haitakuja kuwepo tena! Na itakayokuwepo si kama ile iliyoteketea kwa moto!
KISA CHA MOTO
Mpaka sasa madai ni yaleyale ya awali kuwa, moto huo ulisababishwa na hitilafu ya umeme uliyotokea usiku huo ambao ulianzia kwenye nguzo na kuingia ndani, wanafamilia wakiwa wamelala kwa matumaini ya kuamka asubuhi iliyofuata.
UWAZI KAMA KAWAIDA YAKE
Ni kawaida ya Gazeti la Uwazi punde linapotokea janga zito la kijamii kulifuatilia kwa kina ili kulichimba kwa lengo la kupata yale yasiyopatikana, hivyo timu ya Uwazi ilifika eneo hilo.Hali katika eneo hilo ilikuwa ya ukimya huku baadhi ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali walionekana wakiangalia masalia ya nyumba hiyo. Wengi walikuwa bado wakibubujikwa machozi bila kusema kitu. Kwa kweli tukio hilo limeacha historia ambayo haitasahaulika kamwe kwa wakazi wa eneo hilo.
HALI YA BABA WA FAMILIA KWA SASA
Uwazi baada ya hapo lilimtafuta mzee Masoud, mkuu wa familia hiyo. Yeye amepoteza mke, mama mkwe na watoto wanne. Wengine watatu walioteketea ni ndugu watatu (akiwemo kichanga mmoja) waliotoka Zanzibar.
AWEKWA CHINI YA ULINZI
Mzee Masoud alipatikana Mburahati, Dar ambako alipewa hifadhi na mpwa wake. Alionekana mwenye mawazo mengi na mshtuko wa kila mara. Hata hivyo, aliweza kusimulia tukio zima kwa jinsi alivyopokea taarifa kwa vile yeye alikuwa kazini, lakini huku akiwa chini ya ulinzi mkali wa nduguze ambao walisema wanahofia kumwacha peke yake anaweza kufanya lolote.
Anaanza: “Leo hii sina mtoto hata mmoja! Sina mke wala nyumba. Sijui kama nitakuwa na maisha marefu kuanzia sasa. Nikiikumbuka familia yangu …(anamwaga machozi).“Sijui nimekosea nini Mungu na kuniacha katika hali hii ya upweke. Sina pa kuanzia wala pa kumalizia. Hili ni pigo ambalo sikulitarajia katika maisha yangu (anamwaga machozi tena).”
ALIAGANA NA FAMILIA YAKE VIZURI
“Siku hiyo saa kumi na mbili jioni, niliagana na familia yangu vizuri kwenda kazini. Walinitakia kazi njema wakiamini nitarudi na kuwakuta salama. Nilifika kazini salama, nikaendelea na kazi kama kawaida. Lakini ilipofika saa kumi usiku nilipata simu kutoka kwa jirani yangu mmoja akaniambia nyumbani kuna matatizo hivyo niende.”
ALIFICHWA
“Hata hivyo, yule jirani hakuniambia ni matatizo gani. Nilishtuka sana maana hakuna mtu niliyemwacha mgonjwa. Kabla ya kuamua kuondoka nikampigia simu mke wangu, ikawa hapatikani hewani!
“Nikawapigia watoto nao wakawa hawapatikani. Nilianza kuogopa. Nikaamua kuwapigia ndugu zangu waliokuja kutusalimia wakitokea Zanzibar, nao hawakuwa hewani. Niliingiwa na hofu kubwa, nikawa sina hili wala lile.”
“Nikawapigia watoto nao wakawa hawapatikani. Nilianza kuogopa. Nikaamua kuwapigia ndugu zangu waliokuja kutusalimia wakitokea Zanzibar, nao hawakuwa hewani. Niliingiwa na hofu kubwa, nikawa sina hili wala lile.”
AZUIWA KUFIKA KWAKE
“Baadaye niliomba ruhusa ofisini kurudi nyumbani. Nilipofika karibu na kwangu (Buguruni) nilikutana na baadhi ya majirani. wakanizuia nisifike nyumbani kwa kuniweka sehemu.“Niliwaomba sana waniambie kuna nini nyumbani kwangu mpaka wananizuia nisifike, lakini hawakuniambia. Akili haikuwa na utambuzi wowote na wala sikupata ishara yoyote. Kumbe wakati wananizuia nisifike kwangu ndiyo walikuwa wakitoa mabaki ya miili baada ya kuteketea (analia).”
APEWA TAARIFA, AZIMIA
“Basi, ili kunidhibiti zaidi, nikatolewa pale na kupelekwa kwa ndugu zangu kwingine kabisa. Baadaye ndiyo nikaambiwa kuwa familia yangu niliyoiacha jioni ya watu tisa imeteketea kwa moto ndani ya nyumba na hakuna aliyenusurika. Baada ya taarifa hiyo sikujua kilichoendelea.
“Nilizinduka baadaye nikiwa sijitambui vizuri. Nikasikia familia yangu ilishazikwa. Ina maana ilizikwa bila mimi kuwepo. Lakini pia naamini ningekuwepo na kuona mabaki ya miili yao na mimi leo nisingekuwepo kama wao, ningezikwa nao pamoja (machozi).
“Sina la kufanya, ila nimeumia sana kwani nimepoteza idadi kubwa ya watu kupita kiasi. Leo hii sina watoto, mke, mama mkwe na hata ndugu zangu waliokuja kunisalimia nao wameangamia (machozi tena).
Anamalizia: “Hapa nilipo sijui pa kuanzia wala pa kuishia. Niponipo tu. Kila nikiikumbuka familia yangu nazimia. Hakuna nitakachofanyiwa ili nirudi katika hali yangu ya kawaida zaidi ya familia yangu. Nimeumia sana akili, niacheni nipumzike, sina zaidi ya kuwaambia (machozi tena).”
Anamalizia: “Hapa nilipo sijui pa kuanzia wala pa kuishia. Niponipo tu. Kila nikiikumbuka familia yangu nazimia. Hakuna nitakachofanyiwa ili nirudi katika hali yangu ya kawaida zaidi ya familia yangu. Nimeumia sana akili, niacheni nipumzike, sina zaidi ya kuwaambia (machozi tena).”
MAJIRANI WANASEMAJE
Nao baadhi ya majirani waliohojiana na Uwazi walisema kwamba walisikia kelele usiku saa tisa kutoka ndani ya nyumba hiyo wakihitaji msaada. Walipotoka nje waliona moto mkubwa sana unawaka kwenye nyumba hiyo. Walifika na kujaribu kuvunja mlango mkubwa wa chuma ambao ulikuwa hautumiki na ulifungwa kwa siku nyingi lakini bila mafanikio.
JIRANI AONGEA NA UWAZI
“Ni kweli tulishtuka sana kwani kelele zilizidi kuwa kubwa huku watoto wakisema mamaa…mamaa tuokoe tunakufaa! Bibii…bibii tuokoe tunakufaa... Lakini haikusaidia kwa vile hata mama na bibi nao walikuwa wakipiga kelele za kuomba msaada,” alisema jirani mmoja akijitambulisha kwa jina moja la Musa.
MTOTO MKUBWA
“Baada ya muda tulimuona mtoto mmoja mkubwa wa mzee Masoud, aitwaye Ahmed (pichani) ambaye alikuwa akisoma kidato cha kwanza. Alikuja hadi mlango mkubwa na kututupia funguo ili tuwafungulie kisha akatutupia na kipande cha chuma ili kitumike kubomolea mlango ili aweze kuwaokoa wenzake.
“Alisimama mlangoni kwa muda akitusubiri tuanze uokoaji. Wakati huo moto nao ulikuwa unazidi kushika kasi. Tulijitahidi kadiri ya uwezo wetu lakini hakukuwa na mafanikio kwani geti la chuma lilikuwa na moto sana hivyo kulishika ilikuwa haiwezekani.”
MANENO YA MWISHO YA MTOTO
“Ahmed alipoona hakuna jitihada zozote za kuokolewa, alikata tamaa maana sasa ule moto ulikuwa ukimwangukia maungoni. Akasema: “Basi kama mmeshindwa kutuokoa, acha mimi nirudi kwa bibi na wadogo zangu tukafe kwa pamoja.”
MLIPUKO WAWAKIMBIZA
“Hatukumwona tena Ahmed na kelele ndani zilipungua. Hata hivyo, sisi hatukukata tamaa ya kuwaokoa. Tuliendelea kuvunja mlango lakini ghafla kukasikika mlipuko mkubwa kutoka ndani ya nyumba hiyo. Watu wote tuliokuwa pale tulikimbia vibaya sana. Kuna walioumia kwa kukanyagana kutokana na kukimbia huko.
“Kisa cha kukimbia hatukujua ule mlipuko ulitokana na nini! Ulikuwa kama bomu. Tena baada ya mlipuko huo moto mkubwa uliongezeka na hakuna kelele tena iliyosikika kutoka ndani ya nyumba.
“Baadaye tulirudi eneo la tukio lakini tukiwa na machale. Tulikuta moto umepamba hadi ulipoamua kuacha wenyewe ndiyo tuliweza kuuzima na kukuta familia hiyo imeungua kwa pamoja kwenye chumba kimoja. Inaonekana wakati wanaungua waliamua kushikana. Inauma sana kwa kweli.
“Na kumbe ule mlipuko ulikuwa wa mtungi wa jiko la gesi. Baada ya kupata moto gesi ililipuka na kuchochea ule moto. Baadaye polisi walifika na kuchukua mabaki ya miili na kupeleka Hospitali ya Amana.”
Mjumbe wa Nyumba Kumi Shina Namba 50, Tawi la Malapa, Nassoro Athuman Kicharachara alisema siku hiyo aliamka usiku baada ya kusikia harufu ya kitu kikiungua kama mpira na alipotoka nje aliona moto ukiwaka kwenye nyumba hiyo.
“Ilibidi niwaamshe majirani kwani nilikuwa nikisikia sauti ya kelele kutoka ndani ya nyumba hiyo. Tulikwenda eneo la tukio na kuanza kazi ya uokoaji lakini tulishindwa kutokana na moto kuwa mkubwa,” alisema mjumbe huyo.
MAJINA YA MAREHEMU
Majina ya wanafamilia hao walioteketea kwa moto ni; Samila Juma (mke wa mzee Masoud), Bi. Mdogo Binti Masoud (mama mkwe), Wadha Saleh Zahor (hakufafanuliwa), Samila Haruna (hakufafanuliwa) na mtoto mchanga wa mwaka mmoja na miezi mitatu (jina limesahaulika).
Wengine ni Aisha Masoud (mtoto), Abdillah Masoud (mtoto), Ahmed Masoud (mtoto) na Ashiraf Masoud (mtoto), wote walizikwa katika Makaburi ya Kisutu, Dar, Alhamisi iliyopita.Kwa yeyote aliyeguswa na tukio hilo la majonzi anaweza kuwasiliana kupitia namba 0776 300537, mzee Masoud Mattar Masoud ambaye ndiye mfiwa
BOFYA HAPA KWA KUJIUNGA NASI MOJA KWA MOJA NA LIKE PAGE YETU
HII NI MO DESIGN
Post a Comment
Tafadhali, Usitumie lugha ya matusi! Maoni yako ni ya muhimu sana kwetu.