SERIKALI leo inatazamiwa kujibu hoja mbalimbali zilizoibuka wakati wa mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2015/16.
Mbali
na Wizara ya Fedha ambayo itakuwa na mengi ya kufafanua au kurekebisha
kutokana na mapendezo yake mbalimbali yaliyomo kwenye Bajeti, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Dk Mary Nagu, naye atakuwa na
‘kibarua’ cha kujibu hoja za wabunge kutokana na taarifa yake ya Mpango
wa Maendeleo ya Taifa katika mwaka ujao wa fedha alioiwasilisha bungeni
siku ambayo Bajeti ilisomwa, Juni 11, mwaka huu.
Moja
ya hoja inayotarajiwa kutolewa ufafanuzi au kufanyiwa marekebisho na
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya pamoja na manaibu wake, Adamu Malima na
Mwigulu Nchemba kabla ya Bejeti ya Serikali kupitishwa kwa kupigiwa
kura, ni ongezeko la tozo ya nishati ya mafuta.
Katika
bajeti ijayo, Serikali inapendekeza kuongeza tozo ya mafuta ya dizeli
kutoka Sh 50 kwa lita hadi Sh 100 kwa lita; petroli kutoka Sh 50 hadi Sh
100 kwa lita na mafuta ya taa kutoka Sh 50 kwa lita hadi Sh 150. Kuhusu
mafuta ya taa ilielezwa kwamba ongezeko hilo litasaidia pia kuondoa
uchakachuaji.
Tozo
hiyo ambayo fedha zitakazopatikana zinatarajiwa kupelekwa kwenye Mradi
wa Kusambaza Umeme Vijijini (REA) iliwagawa wabunge katika makundi
mawili; moja likiipinga na lingine likiiunga mkono.
Wale
wanaopinga wanasema itaongeza mzigo kwa wananchi kwa kuwa nishati hizo
zinapoguswa zina athari nyingi za kuendelea lakini wale wanaounga mkono
tozo hiyo wanasema ni ndogo kulinganisha na umuhimu wake na kwamba
maendeleo hayawezi kuja bila kuyatolea jasho.
Suala la nyongeza pensheni nalo linatarajiwa kutolewa ufafanuzi wa Wizara.
Serikali
katika mwaka ujao wa fedha inapendekeza kiwango cha pensheni kupanda
kutoka Sh 50,000 za sasa hadi Sh 85,000. Hata hivyo, wabunge wengi
walitaka kiwango hicho kiongezeke hadi kufikia Sh 100,000 au zaidi huku
wachache wakisema hizo zilizopendekezwa zinatosha.
Wizara
hiyo ya Fedha pia itajaribu kujibu hoja kwamba bado kuna vyanzo vya
mapato vingi kama uvuvi kwenye bahari kuu ambako tumeshindwa kwenda na
kwamba kwenye migodi na utalii tungeweza kupata mapato mengi zaidi
kuliko ilivyo sasa.
Wizara
hiyo pia itajaribu kueleza namna itakavyodhibiti matumizi katika mwaka
ujao wa fedha kwani baadhi ya wabunge walilalamikia kukosekana kwa
nidhamu ya pesa kwenye taasisi nyingi za umma huku hatua za
kuwawajibisha watuhumiwa zikiwa legelege.
Mbali
na mikakati iliyopo katika kuimarisha Shilingi, serikali itatakiwa pia
kujibu namna takavyoshughulikia madeni yake kama vile makandarasi,
mifuko ya hifadhi ya jamii hadi wakulima wanaoidai serikali takribani Sh
bilioni 22.
Waziri
Nagu naye atatakiwa kujibu hoja kwamba ingawa uchumi unaonekana kukua
kwa asilimia 7 na hivyo kuifanya Tanzania kuwa kati nchi 20 duniani
zenye mwelekeo mzuri wa uchumi, hali hiyo haijitafsiri vyema katika
mifuko ya wananchi.
Wizara
ya Viwanda nayo, kati ya hoja kadhaa zilizoelekezwa huko, italazimika
kueleza ni jinsi gani imejizatiti katika kuimarisha viwanda nchini na
kuhamasisha wawekezaji zaidi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa zenye
uhitaji mkubwa nchini kama pikipiki na bajaji na hivyo kukuza uchumi na
kutengeneza ajira zaidi.
Baadhi
ya wabunge walikuwa na hoja kwamba ni wakati sasa wa kuimarisha na
kujenga viwanda nchini, ili tusiendelee kuwa nchi ya kuagiza kila kitu
hadi madodoki, hali ambayo inatufanya tuhitaji sana matumizi ya dola na
hivyo kuyumbisha thamani ya Shilingi yetu.
Wizara
ya Kilimo nayo itatakiwa kujibu hoja zilizoelekezwa kwake, hususani
namna itakavyojipanga kuhakikisha Tanzania inakuza kilimo chake ikiwa ni
pamoja na kuuza mchele katika nchi jirani ikiwemo Kenya ambayo
inapeleka pesa zake za kigeni Pakistan ili kupata zaidi ya kilo laki
mbili za mchele kila mwaka.
Wakati
karibu kila wizara iliguswa na mjadala, Ofisi ya Waziri Mkuu pia
itatakiwa kujibu namna itakavyosimamia ulipaji wa fidia kwa halmashauri
zilizopata ‘maafa’ kama ile ya Masasi iliyochomwa moto na wahuni pamoja
na upatikanaji wa rasilimali fedha katika halmashauri mbalimbali nchini
utakaokuwa unakwenda kwa wakati.
Wakati
akiahirisha Bunge Ijumaa iliyopita, Sipika Anne Makinda alivitaka vyama
vyote vya siasa kuhakikisha wabunge wao wanakuwepo leo ili kusikia
majibu ya serikali.
Wiki iliyopita wakati wa majadiliano ya Bajeti ya Serikali na Hali ya Uchumi kulikuwa na mahudhurio yasiyoridhisha ya wabunge na mawaziri.
Wiki iliyopita wakati wa majadiliano ya Bajeti ya Serikali na Hali ya Uchumi kulikuwa na mahudhurio yasiyoridhisha ya wabunge na mawaziri.
BOFYA HAPA KWA KUJIUNGA NASI MOJA KWA MOJA NA LIKE PAGE YETU
HII NI MO DESIGN
Post a Comment
Tafadhali, Usitumie lugha ya matusi! Maoni yako ni ya muhimu sana kwetu.