IKIWA tayari Ubalozi wa Ubelgiji nchini
Tanzania umekwishatoa viza kwa mshambuliaji Mbwana Samatta kwenda
kusaini klabu ya KRC Genk, lakini taarifa zinasemekana kuwa huenda
anaweza akabaki TP Mazembe ya DRC kumalizia Mkataba wake hadi Aprili.
Hiyo inatokana na Rais wa Mazembe, Moise
Katumbi kugoma kumuuza Mwanasoka huyo Bora wa Afrika kwa wachezaji wa
ndani katika klabu hiyo Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Inasemekana pia kuwa, Katumbi anataka
Samatta anende kucheza Nantes FC ya Ligi Kuu ya Ufaransa, ambayo
amekwishafikia makubaliano nayo, na kwamba wiki iliyopita Nantes FC
ilituma mwakilishi wake jijini Dar es Salaam, ambaye alifanya mazungumzo
na Meneja wa Samatta, Jamal Kisongo mbele ya Ofisa mmoja wa Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF).
Katika mazungumzo, Kisongo alifikia
makubaliano ya maslahi binafsi na Samatta ikiwemo dau la kusaini,
mshahara, masharti na marupurupu mengine. Kisongo alitaka kiwepo
kipengele cha mchezaji kutorejeshwa Afrika iwapo hatapata nafasi ya
kucheza Nantes, bali auzwe klabu nyingine ya Ulaya na ikakubaliwa.

Nantes ilionesha nia ya dhati kabisa ya
kumchukua Samatta na Kisongo aliinuka kwenye meza ya mazungumzo akiwa
amekubali na kusema anakwenda kuzungumza na mchezaji. Hata hivyo,
inaonekana Samatta mwenyewe ndiye anayetaka kwenda Ubelgiji na si
Ufaransa, kwani kitendo cha Kisongo kutorejesha majibu kwa Nantes
kinaashiria ameshindwa kumshawishi mchezaji wake akubali ofa hiyo.
Wakati huo huo, Rais wa Mazembe hayuko
tayari kumuuza Samatta Ubelgiji na yuko tayari kuona Samatta anabaki
Mazembe kumalizia Mkataba wake ili aondoke kama mchezaji huru Aprili,
hali ambayo itamlazimu kusubiri hadi Agosti kusaini Genk.
Kwa sasa, kambi ya Samatta inajaribu
kuomba msaada kwa viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, wakazungumze na Katumbi ili akubali kumuacha mchezaji aende
klabu aliyochagua.
Rais Mstaafu, Dk Jakaya Mrisho Kikwete
ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa chama tawala, CCM, Waziri wa Michezo,
Nape Nnauye kwa pamoja wameahidi kumsaidia Samatta katika suala la
kumlainisha Katumbi akubali kupokea ofa ya Genk.
Wakati huo huo, Nantes wamekuwa
wakimpigia simu Kisongo wakisema wanamsubiri mchezaji aende kusaini,
lakini Meneja huyo anakosa majibu ya uhakika.
Inaonekana tayari Katumbi anaujua mchezo
wote unaoendelea naye ameamua kukaa kimya akiamini Samatta hawezi
kufanya chochote kwa sasa bila baraka zake. Wazo la kusema Samatta
asubiri hadi mwezi Aprili atakapomaliza Mkataba wake ili kusaini kama
mchezaji huru mwezi Agosti, halifurahiwi hata na Kisongo mwenyewe.
Samatta aliyejiunga na TPM mwaka 2011
akitokea Simba SC aliyoichezea kwa nusu msimu, akitokea African Lyon,
hadi sasa ameichezea klabu hiyo mechi 103 na kuifungia mabao 60. Ndani
ya mechi hizo, kijana huyo wa umri wa miaka 24, ameshinda taji la Ligi
ya Mabingwa Afrika na Mazembe, huku naye akiibuka mfungaji bora wa
michuano hiyo na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Afrika.
BOFYA HAPA KWA KUJIUNGA NASI MOJA KWA MOJA NA LIKE PAGE YETU
HII NI MO DESIGN
Post a Comment
Tafadhali, Usitumie lugha ya matusi! Maoni yako ni ya muhimu sana kwetu.