Miili ya majambazi hao ikiwa ndani ya gari la polisi.
Stori: Issa Mnally na Makongoro Oging’, UWAZI
DAR ES SALAAM!
Simulizi ya majambazi kuvamia Benki ya Access iliyopo Mbagala ya Rangi
Tatu jijini Dar, Ijumaa iliyopita bado inasikika miongoni mwa jamii
ikisema ilikuwa vita kamili huku masikitiko makubwa yakiwa kwa watu
watano waliouawa ukiweka kando majambazi watatu ambao waliuawa na
polisi.
TIMU YA UWAZI ENEO LA TUKIO
Kawaida ya Gazeti la Uwazi, ni kuchimba
mambo ambapo waandishi wake walifika eneo la tukio muda mfupi baada ya
kutulia kwa milio ya risasi huku sehemu kubwa ya polisi wakiwa
wamewafuata majambazi hao.
SIMULIZI YA MAJIRANI WA BENKI
Uwazi lilianza kwa kuongea na baadhi ya
wafanyabiashara wenye maduka yaliyo jirani na benki hiyo ambapo
walisimulia kile walichokiona.
“Sisi tulishtuka kusikia milio ya
risasi. Ndipo tulipobaini kuwa ni majambazi. Walifunga barabara kwa
kumimina risasi hovyo ambapo magari kutoka kusini na yale yaliyokuwa
yakitoka Posta na Kariakoo yalishindwa kupita na hakukuwa na mtu yeyote
aliyekuwa akikatisha maeneo haya,” alisema jirani mmoja.
Hali ilivyokuwa baada ya tukio hilo la kutisha.
ALIANZA KUINGIA MWANAMKE
Hamis, mmoja wa majirani wa benki hiyo
aliyekoswakoswa risasi, alisimulia alichokiona mwanzo hadi mwisho ambapo
alikuwa na haya ya kusema:
Wananchi wa Mbagala wakitaharuki baada ya tukio hilo.
“Ile ilikuwa ni vita kabisa! Ni vita
jamani si ujambazi ule. Ilikuwa majira ya saa nane na nusu, nilimwona
mwanamke mmoja akiingia benki. Huyu mwanamke nasikia ndiye alikuja
kufanya ukaguzi wa mwisho. Alikuwa kundi moja na majambazi.
Gari lililopigwa risasi kwenye kioo chake.
“Hata hivyo, tuliambiwa kuwa baadhi ya
wateja walimshtukia mwanamke huyo kwa sababu alipoingia, alisimama,
akaangaza-angaza na kutoka. Wateja waliwaambia askari wa kampuni binafsi
inayolinda hapa benki kwa kushirikiana na polisi wamhoji kwani
aliashiria si mtu mzuri.
Hali ilivyokuwa ndani ya benki hiyo.
BUNDUKI NDANI YA MKEKA
“Lakini kabla hatua hizo hazijafanyika, ghafla nilimwona mwanaume mmoja amebeba mkeka wa China akiwa ameukunja.
“Alipokaribia, aliuweka chini mkeka huo
na haraka sana akatoa bunduki moja aina ya SMG na kumfyatulia risasi
polisi aliyekuwa na bunduki, Haridi Juma (28), kisha akarusha nyingine
kwenye banda lao ambapo kulikuwa na polisi mwingine ambaye alijeruhiwa
na akachukua bunduki zao.
WAONGEZEKA
Hali ya taharuki ilitokea, ndipo
nikaona majambazi wengine wakiongezeka na kuingia ndani ya benki sasa
ambapo walimuua kwa risasi mlinzi wa kampuni binafsi.”
Ofisa wa Polisi aliyeuawa (enzi za uhai wake).
WENGINE WALIOUAWA KWA RISASI
Taarifa zinasema kuwa wengine waliouawa
kwa kupigwa risasi na majambazi hao, ni kijana mmoja aliyekuwa akiuza
vinywaji baridi pembeni ya benki hiyo, aliyekuwa akifahamika zaidi kwa
jina la Mgosi. Inadaiwa kisa cha kupigwa risasi ni kitendo chake cha
kupiga kelele akisema: ‘Wezi hao! Majambazi hao!’
Jeneza lenye mwili wa askari huyo likiwa ndani ya gari la polisi.
Pia kuna mwanamke mmoja yeye alikuwa akitoka ndani ya benki hiyo na kukumbana na majambazi.
Naye mfanyakazi mmoja wa benki hiyo ambaye hakupenda kutaja jina lake, akisimulia sakata hilo, alisema:
“Ilikuwa vita! Mimi nilishangaa kuona
kioo cha mlango kinamwagika chini sambamba na mlio wa risasi. Nikaona
watu wameingia ndani wakiwa na bunduki. Ni tukio baya sana kulishuhudia.
“Humu
ndani walikwenda kujaribu kuvunja mlango wa chumba maalum cha
kuhifadhia kiasi kikubwa cha fedha (strong room) lakini wakashindwa
ndipo wakachukua zilizokuwepo kwenye droo nyingine. Kwa kweli hali
ilikuwa mbaya sana, milio ya risasi ilitawala kila kona, watu tulikuwa
tumelala kwa amri ya majambazi.
“Walisema atakayepingana na amri yao watampiga risasi na kumuua. Sikumbuki hata kama nilikumbuka kusali kwa Mungu wangu.
jeneza lenye mwili wa askari likipandishwa kwenye gari tayari kwa kuelekea Mkoani Tanga kwa ajili ya mazishi.
POLISI WAFIKA
“Hata hivyo, haikuchukua muda polisi
wakafika na kupambana nao kwa kurushiana risasi. Gari la polisi
lilishambuliwa kwa risasi. Unajua kilichotokea ni kwamba polisi wao
walikuwa wakirusha risasi kwa tahadhari wasiwadhuru wananchi, majambazi
walikuwa wakizimimina kama mvua.”
Mfano wa bomu lililotumiwa na majambazi hao.
SHUHUDA WA NJE
Jerry Milo ni mmoja wa wakazi wa eneo
hilo, yeye alishuhudia vita yote mwanzo hadi mwisho. Alisema kuwa,
jambazi mmoja aliyesimama barabarabni ndiye aliyekuwa na jukumu la
kuzuia magari kupita eneo hilo.
Alisema: “Yule jambazi alikuwa na
bunduki mbili. Alikuwa akifyatua risasi juu, nyingine upande wa magari.
Alipoliona Defender la polisi akalifyatulia risasi, ikaingia kwenye kioo
cha mbele lakini haikumpata mtu, Defender likaingia mtaroni.
MWANAJESHI ATAJWA
“Sasa hapo majambazi walishatoka benki na pesa. Wakaanza kukimbia wakiwa na bodaboda sita. Kila bodaboda walipanda wawili.
“Mwanajeshi mmoja wa JWTZ (Jeshi la
Wananchi wa Tanzania) alitokea akiwa amevaa sare, akamfuata polisi
mmoja, akamwonesha kitambulisho, akamwambia ampe bunduki, akapewa. Kazi
ikawa kuwawahi wale majambazi maana walishaondoka na polisi wengine
walikuwa wakiwafuata kwa nyuma.
BODABODA ROHO REHANI
“Suka (dereva) mmoja wa bodaboda
aliyekuwa akipita maeneo hayo akienda Bunju baada ya kumpeleka mteja,
alimuuliza yule mwanajeshi kama anaweza kupambana na majambazi hao
apande pikipiki yake wawafukuze.
“Mjeshi akasema anaweza, akapanda.
Alimwambia jamaa wa bodaboda kwamba akimgusa upande wa kulia alalie
huko, akimgusa kushoto alalie hukohuko, nadhani ili apate nafasi ya
kuelekeza mtutu wa bunduki mbele.”
MPAKA KIJIJI CHA CHURWI
Habari zinasema kuwa polisi kwa
kushirikiana na mwanajeshi huyo waliwakimbiza majambazi hao mpaka kwenye
Kijiji cha Churwi kilichopo Wilaya ya Mkuranga, Pwani ambako waliwaua
watatu baada ya kurushiana risasi, tisa wakatokomea huku wakitelekeza
pikipiki zao na bunduki tatu. Miongoni mwa waliouawa, mmoja alikutwa na
hirizi shingoni.
KAULI YA KAMANDA WA POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, ACP
Andrew Satta na kikosi chake wamekuwa katika oparesheni kali kwenye Pori
la Mkuranga kwa siku zote na juzi aliliambia gazeti hili kuwa
atahakikisha wahusika wote wanapatikana na kambi yao kusambaratishwa.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI ATOA TAMKO
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles
Kitwanga alisema amewasiliana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Dk. Hussein Mwinyi ili apate ushirikiano kutoka JWTZ lililo chini
ya mkuu wake, Jenerali Davis Mwamunyange ili kufanyike oparesheni ya
nguvu katika misitu ya Mkoa wa Pwani ambako inaaminika kuna makundi ya
majambazi.
Mwili wa marehemu Haridi ulisafirishwa Jumamosi iliyopita kwenda kwao Tanga kwa mazishi
BOFYA HAPA KWA KUJIUNGA NASI MOJA KWA MOJA NA LIKE PAGE YETU
HII NI MO DESIGN
Post a Comment
Tafadhali, Usitumie lugha ya matusi! Maoni yako ni ya muhimu sana kwetu.